Kiungo wa Simba Jonas Mkude hajaonekana kwa muda uwanjani, huku ikielezwa pia mkataba wake upo ukingoni kabla ya kumalizika na kuleta hofu kwa mashabiki na wanachama wa Simba, lakini mwenyewe amevunja ukimya na kuwatuliza akiwaambia bado yupo sana Msimbazi
Mkude amekuwa hana nafasi ya uhakika kwenye kikosi cha Juma Mgunda, lakini mwenyewe amesema kutokuonekana kwake kumetokana na kuwa majeruhi na hata alivyorudi hakuwa fiti tofauti na wachezaji waliochukua nafasi yake kikosini.
Kiungo huyo mkabaji ambaye ni mwandamizi kwenye kikosi cha sasa cha Simba, alisema kwa sasa yupo fiti tayari kuliamsha kikosini na kufichua ishu ya mkataba wake alisema wanapaswa kuulizwa na viongozi wa timu
"Kuna muda nilipata majeraha, sikuweza kufanya mazoezi na timu na hata nilivyopona ilihitaji muda pia ili kurudi kwenye utimamu kama wenzangu ndio maana mara nyingi nilikuwa sionekani uwanjani na muda mwingine naanzia benchi," alisema Mkude na kuongeza
"Kwa sasa niko poa na tayari kwa mapambano nadhani kilichobaki ni kwa benchi la ufundi kuamua kunitumia"
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba Juma Mgunda alisema Mkude ni mchezaji mzuri na yupo Simba ili kuhakikisha inatimiza malengo hivyo yupo kwenye mipango yake na atamtumia kutokana na matakwa ya mchezo husika
"Ni mchezaji mwenye uzoefu wa kutosha, anastahili kuichezea Simba na nitamtumia kutokana na uhitaji wa mechi kwani yupo hapa ili kuitumikia timu," alisema Mgunda
Mwanaspoti