Mshambuliaji mpya wa Singida Big Stars, Ibrahim Ajibu baada kupewa stahiki zake zote na uongozi wa timu hiyo uliomsajili kwa mkataba wa miaka miwili, alijiunga na kikosi asubuhi ya jana.
Ajibu alitua kwenye kambi ya timu hiyo kishua kwani aliondoka Dar es Salaam kwa ndege hadi Dodoma na baada ya kufika hapo kulikuwa na gari maalumu aliloandaliwa na kumfikisha Singida.
Baada ya kufika Singida alipewa nyumba yake binafsi aliyoandaliwa kuishi hapo kwa muda wote ambao atakuwa ndani ya kikosi hicho wakati timu ikiwa haipo kambini.
Bado uongozi wa Singida Big Stars haujaweka wazi suala la kumalizana na Ajibu ila huenda akawepo katika moja ya mechi za Ligi Kuu Bara kati ya Dodoma Jiji au dhidi ya Geita Gold, ambao baada ya hapo watakwenda kwenye Kombe la Mapinduzi Zanzibar.
Ajibu atakuwa mchezaji wa pili kutambulishwa kwenye kikosi hicho baada ya beki wa kushoto, Nickson Kibabage aliyesajiliwa kutokea Mtibwa Sugar kama ambavyo Mwanaspoti lilikueleza hapo awali.
Alipotafutwa Ajibu alisema timu yake mpya ndio yenye mamlaka ya kueleza usajili wake ila kwa sasa yupo kwenye hatua za mwisho kujiunga nao.
“Wala usiwe na haraka siku si nyingi mashabiki wangu wataniona uwanjani nikiwa kwenye majukumu ya timu nyingine,” alisema Ajibu aliyewahi pia kucheza Simba, Yanga na Azam FC.